• Latest News

  Monday, April 28, 2014

  Fuko, mnyama hatari kwa mazao yako .Mwenye madhara makubwa sana  Fuko ni aina ya mnyama mdogo anayeishi chini ya ardhi kwenye mashimo. Mnyama huyu hutumia kiwango kidogo sana cha hewa ya oksijeni. Fuko hupatikana sehemu za wazi ambazo hazina misitu minene, na zenye mazao kama vile viazi.


  Fuko
  Udongo uliorundikana shambani ni dalili za uwepo wa fuko.
  Fuko huzaliana mara 4 kwa mwaka wakati mnyama mmoja huzaa watoto 4-6. Ambapo hujenga nyumba yake chini ya ardhi ambako si rahisi kwa adui kumfikia. Mnyama huyu hujenga shimo lake kwa ustadi mkubwa kiasi cha kuwa na sehemu ya kulala, stoo ya chakula, mahali pa starehe, sehemu ya choo, na sehemu ya kujificha adui anapotokea.


  Kwa miaka mingi fuko wamekuwa tatizo kwa wakulima, hasa katika baadhi ya mikoa ambayo huzalisha mazao yenye tunguu au viazi. Baadhi ya mikoa hiyo ni Kagera, Arusha na Kilimanjaro, ambapo hupatikana maeneo yote ya miinuko na tambarare.


  Lishe


  Fuko hula mizizi ya mazao na sehemu ya chini ya shina la mmea husika pamoja na mazao yenyewe, kama vile viazi. Hali hii husababisha mimea kufa na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa mkulima.
  Wanyama hawa hula aina zote za mazao, na huhifadhi chakula kwa ajili ya msimu wa kiangazi. Kila mmoja wao huhifadhi kiasi cha debe mbili kwa matumizi ya wakati huo.


  Fuko mmoja mkubwa huweza kula kiasi cha gramu 50-60 za chakula kwa muda wa siku moja. Kwa hivyo humsababishia mkulima hasara hata kufikia asilimia mia moja.


  Aina


  Fuko 1
  Hii ni aina moja ya fuko walio katika umri tofauti wakiwa wamenaswa.
  Kimtazamo, fuko hunekana kuwa aina mbili. Lakini kulingana na utafiti uliofanyika mkoani Kagera wanyama hawa ni wa aina moja tu. Mwenye rangi nyeusi ni fuko wa umri mdogo na mwenye rangi ya kahawia ni mkubwa na anaelekea kuzeeka.


  Mazao yanayoharibiwa zaidi na fuko

  Fuko hula aina zote za mazao, ingawa kuna baadhi ambayo huliwa zaidi na kusababisha hasara kubwa kwa mkulima. Haya ni baadhi tu ya mazao yanayoliwa zaidi: Mihogo, viazi vitamu, viazi mviringo, maharagwe, magimbi, miwa, mahindi, na karoti.


  Mazao mengine huharibiwa lakini haya ni kwa kiwango cha juu zaidi, ambapo humuacha mkulima akiwa amepata hasara kubwa na mara nyingine bila kuvuna hata kidogo. Wanyama hawa hawanywi maji, badala yake hupata kutoka kwenye mazao wanayokula.

  Namna wanavyoharibu

  Fuko anapokuwa mdogo, hula mimea michanga tu. Anapokuwa mkubwa hula mimea iliyokomaa, na kisha kuhifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye.


  Namna ya kudhiti fuko shambani

  Kuna njia nne zinazoweza kutumika kudhibiti wanyama hawa waharibifu.


  Mimea: Baadhi ya mimea imekuwa ikitumika kama chambo kudhibiti fuko, lakini njia hii imeonekana kutokuwa na ufanisi mkubwa sana.
  Kemikali: Haishauriwi kutumia njia hii kwa kuwa ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu pia.
  Kutega: Inapendekezwa kutumia njia hii kwa kuwa imeonekana kuwa na ufanisi mkubwa.
  Kupiga: Hii ni njia sahihi pia, japo ufanisi wake ni mdogo ukilinganisha na kutega.


  Aina za mitego
  Fuko 3
  Tutumia mitego kuangamiza fuko kuliko aina nyingine ya udhibiti.
  Fuko 2
  Weka mtego kwenye shimo la fuko kisha funika kwa ustadi.
  Kuna aina nyingi za mitego inayotumika kukamata fuko, hii hutegemea na aina na maeneo na jamii husika. Ifuatayo ni baadhi ya mitego ambayo imeonekana kuwa na ufanisi.


  • Waya • Boksi • Ubao


  *Inashauriwa wakulima kutotumia sumu kukabili wanyama hawa, kwani aina ya sumu inayoweza kuwaua wanyama hawa ni kali na hatari kwa afya.


  Endapo utavuta hewa ya sumu hii, unaweza kupoteza maisha baada ya muda mfupi sana. Halikadhalika, sumu hii ni hatari kwa mazingira, mimea, na viumbe wengine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Fuko, mnyama hatari kwa mazao yako .Mwenye madhara makubwa sana Rating: 5 Reviewed By: Kilimo mifugo
  Scroll to Top