• Latest News

  Friday, September 12, 2014

  AFYA YAKO: TATIZO LA KUHARIBIKA MIMBA MARA KWA MARA


  Tatizo la kuharibika mimba mara kwa mara kitaalamu huitwa ‘Recurrent pregnancyloss’. Mwanamke hujitahidi kutafuta ujauzito lakini inakuwa ngumu ujauzito kukua hadi kufikia kujifungua.
  Hali hii huleta athari kubwa kwa mwanamke pamoja na kuathirika kiafya kutokana na mimba kuharibika mara kwa mara lakini pia huathirika kisaikolojia kwa kutopata watoto. Ni mojawapo ya tatizo linalochangia ugumba katika jamii.

  Kipindi cha ujauzito huchukua majuma arobaini kuanzia mimba inapotungwa hadi mama anakuja kujifungua mtoto kamili.  Mtoto kamili na mwenye afya njema huzaliwa katika uzito wa kilo kuanzia mbili na nusu.

  Chini ya uzito huu ni watoto wenye matatizo na wanakuwa katika uangalizi maalumu hospitali chini ya usimamizi wa madaktari wa watoto.Kipindi cha ujauzito pia kimegawanyika katika vipindi vitatu ambavyo kitaalamu huitwa ‘Trimesters’, vipindi hivi ni vya miezi mitatu mitatu.  Miezi mitatu ya kwanza tunaita kipindi cha uumbaji.

  Katika kipindi hiki ndipo viungo vya mtoto vinapoumbwa na kukamilika.Mimba inayoumbwa ikiwa na kasoro mwili wa mama unaofanya kazi vizuri huitoa wenyewe, hapa ndipo tunapopata historia ya mama kwamba amepoteza mimba kadhaa zikiwa na umri wa chini ya miezi mitatu. Ni mara chache vyanzo vyake kutibika.

  Vipo vyanzo vingi vinavyosababisha mimba changa ziwe zinatoka, vyanzo hivi ni rahisi kugundulika baada ya kuhudhuria hospitali kwa daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi.
  Ujauzito kuharibika katika miezi mitatu ya kwanza chanzo ni mimba yenyewe.

  Ujauzito kuharibika katika miezi mitatu ya pili hutokana na tatizo katika mlango wa kizazi wa mama kushindwa kushikilia mimba. Tatizo hili kitaalamu huitwa ‘cervical incompetence’.

  Mama anakuwa na historia ya mimba kumtoka kuanzia umri wa zaidi ya miezi mitatu hadi sita.  Mimba inaendelea vizuri kwa zaidi ya miezi mitatu ya kwanza na inapofikia miezi mitatu ya pili inatishia kutoka hadi inatoka.

  Vyanzo vya mlango wa kizazi kulegea vipo vingi navyo pia vinahitaji uchunguzi wa kina kwa daktari wa kinamama na ikithibitika hivyo, basi mlango wa kizazi utashonwa na mama atapata mapumziko ya muda mrefu na akija kujifungua atafunguliwa kwanza nyuzi kisha atajifungua.

  Katika kipindi hiki hata mtoto anaweza kufia tumboni na chanzo kikuu kinaweza kuwa upungufu mkubwa wa damu kwa mama mjamzito, shinikizo la damu kuwa juu na sababu nyingine ambazo daktari atazigundua.

  Kwa kawaida presha ya mama mjamzito inatakiwa isizidi 120 kwa 80.  Ikizidi hapo ni vema ufuatilie kwa daktari wako.

  Shinikizo la damu kuwa juu kwa mama mjamzito dalili zake ni kuvimba miguu, kukosa pumzi wakati wa kutembea, maumivu ya kifua na wakati mwingine macho hayaoni vizuri, akipimwa mkojo ataambiwa kuna protini nyingi kwenye mkojo.

  Presha ikizidi kupanda, basi mama mjamzito atapata kifafa cha mimba. Pamoja na dalili hizo, ataanza kurusharusha mikono na miguu na kuwa kama mtoto mwenye degedege au mgonjwa wa kifafa.
  Ni dalili ya hatari kwa uhai wa mama na mtoto.

  NINI CHA KUFANYA?
  Matatizo ya kuharibika kwa mimba mara kwa mara au watoto kufia tumboni ni tatizo linaloathiri afya ya mama na jamii yake kwa ujumla kwa kila kitu.Kama nilivyoelezea hapo awali, tatizo hili lina ufumbuzi endapo mama atahudhuria hospitali mapema. Uchunguzi na tiba hupatikana katika hospitali za wilaya na mikoa popote nchini.

  Muone daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na matatizo ya uzazi katika hospitali hizo. Epuka imani potofu katika masuala haya, fuatilia uchauri wa kidaktari
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: AFYA YAKO: TATIZO LA KUHARIBIKA MIMBA MARA KWA MARA Rating: 5 Reviewed By: Kilimo mifugo
  Scroll to Top