• Latest News

  Monday, October 20, 2014

  KILIMO NA HIFADHI BORA YA VITUNGUU


  1. UTANGULIZI

     Vitunguu ni zao muhimu sana hapa Tanzania. Mikoa ya Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya,
  Tanga, Singida na Kilimanjaro ni maarufu sana kwa kilimo cha vitunguu na ni zao la chakula na
  biashara kwa mkulima mdogo. Uzalishaji wa vitunguu bado ni mdogo (tani nne kwa hekta) na
  upotevu wa mazao baada ya kuvuna ni mkubwa (50 %– 80%) kutokana na hifadhi duni hivyo
  wakulima wanahitaji utaalamu wa kilimo bora na hifadhi ya vitunguu ili kuongeza uzalishaji na
  kipato.

  2.0 Uzalishaji wa vitunguu
  Zao la vitunguu linazalishwa kutokana na mbegu na miche inakuzwa kwenye kitalu kabla ya
  kupandikizawa shamban. Miche inakuwa na kuzaa vitunguu.Vitunguu vikikomaa, vinavunwa na
  kuhifadhiwa vikiwa katika hali ya kulala bwete. Katika hali hii vitunguu vinaweza kuhifadhiwa
  kwa muda mrefu aitha kwa ajili ya kuzalisha mbegu msimu unaofuata au kuuza.
  Wingi na ubora wa zao la vitunguu hutegemea; hali ya hewa, aina ya vitunguu, upatikanaji wa
  mbegu bora, kilimo bora, uangalifu wakati wa kuvuna, usafirishaji na hifadhi bora.

  2.1 Uzalishaji
  Hali ya hewa na maji
  Hali ya hewa na maji ni vipengele muhimu sana vya kuzingatia katika uzalishaji wa vitunguu.
  Vitunguu vinastawi vizuri katika hali ya ukavu kwa kutumia umwagiliaji. Maji mengi hasa
  wakati wa masika inasababisha magonjwa mengi hasa ukungu, vitunguu haviwezi kukomaa
  vizuri, hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mazao. Jua na hewa kavu ni muhimu sana wakati
  wa kukomaa na kuvuna vitunguu.
  Aina za vitunguu
  Aina bora za vitunguu ni pamoja na Mang’ola red, Red creole na Bombay Red. Hizi ni mbegu
  bora ambazo zinatoa mazao mengi kuanzia 40-60kgs kwa hekta ikiwa kilimo bora
  kitazingatiwa.Mkulima anaweza kuchagua mbegu kwa kuzingatia:-
  · mahitaji ya soko (vitunguu vyekundu hupendwa zaidi)
  · musimu wa kupanda
  · uwezo wa kuzaa mazao mengi
  · uwezo wa vitunguu kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
  Mbegu bora
  Ubora wa mbegu ni muhimu sana, kwani ndiyo chanzo cha mazao bora. Mbegu bora inatoa
  miche yenye afya na kuzaa mazao mengi na bora. Mbegu za vitunguu inapoteza uoto wake upesi
  baada ya kuvunwa (mwaka1). Mbegu nzuri zina sifa zifuatazo:-
  · Uotaji zaidi ya 80%
  · Mbegu safi zisiyo na mchanganyhiko
  · Zimefungwa vizuri kwenye vyombo visivyopitisha hewa na unjevu.

  Hivyo mkulima anaponunua mbegu za vitunguu azingatie yafuatayo:
  · Chanzo cha mbegu
  · Tarehe ya uzalishaji
  · Tarehe ya kuisha muda wake
  · Kifungashio cha mbegu.
  Inashauriwa mkulima asipande mbegu zenye umri zaidi ya mwaka mmoja
  Mbegu bora za vitunguu zinauzwa na makampuni binafsi kama: ALPHA Seed Co., Popvriend,
  Rotian Seed, Kibo Seed, East African Seed Company nk. Wasambazaji wa mbegu ni pamoja na
  maduka ya TFA, na maduka ya bembejeo za kilimo katika maduka mbalimbali.
  Jinsi ya kuandaa kitalu na kuzalisha miche
  · Sehemu ya kitalu iwe wazi, mbali na kivuli na kiwe karibu na chanzo cha maji.
  · Tengeneza tuta la kubwa wa 1m x 2m . Urefu na idadi ya matuta hutegemea kiasi cha
  mbegu. Kiasi cha mbegu kwa hectare moja ni kilo 6 au 2 kg kwa eka.
  · Weka samadi iliyooza vizuri kiasi cha debe moja au mchanganyiko wa mbolea ya TSP na
  CAN (200gm) kwa uwiano wa 1:1 kwenye tuta changanya vizuri na udongo.
  · Sia mbegu kwenye mistari kwa nafasi ya 1 sm x 20 sm. Tawanya mbegu vizuri wakati
  wa kusia ili miche isisongamane.
  · Funika mbegu na weka matandazo ya nyasi kavu juu ya tuta na mwagiliwa maji. Udongo
  unatakiwa kuwa na unyevu kiasi mpaka mbegu ziote.
  · Nyasi ziondolewe mara tu mbegu zikiota (siku7-10 kutegemea hali ya hewa).
  · Miche itunzwe vizuri na kitalu kiwe katika hali ya usafi.
  · Miche imwagiliwe maji mpaka ifikie umri wa kupandikiza shambani (wiki 5-6)
  Matatizo ya miche kitaluni ni kama yafuatayo:
  Kuonza kwa mbegu, kunyauka kwa miche kabla na baada ya kuoto. Hali hii inasababishwa na
  ugonjwa wa ukungu “Kinyausi” .Dawa za ukungu kama Dithane M45 au Ridomil MZnk
  zinatumike kuzuia (changanya dawa na povu la sabuni ili dawa ijishike kwenye majani). Pia
  uangalifu uwepo wakati wa kumwagilia maji. Mwagilia maji wakati wa asubuhi au jioni. Epuka
  kumwagilia maji wakati wa jua kali kwani unjevunjevu hewani unaongeza na kusababisha
  vimelea vya magonjwa.
  Wadudu waharibifu ni pamoja na Chawa wekundu.ambao wanashambulia majani, Sota ambao
  hukata miche. Dawa za viwandani kama Thiodan , Selecron au Dusrban zinazuia na kudhibiti
  hwa wadudu.
  Baada ya wiki 5 au 6, kutegemeana na hali ya hewa miche itakuwa tayari kupandikiza
  shambani. Miche iimarishwe kwa kusitisha maji, wiki moja kabla ya kupandikiza.
  Kutayarisha shamba
  Shamba litayarishwe sehemu usiyokuwa na mwinuko, sehemu ya wazi ambayo haijalimwa
  vitunguu kwa muda wa miaka 2 -3. Shamba liwe karibu na chanzo cha maji kwa ajili ya
  umwagiliaji. Matuta 1m x 3m au majaruba ya 2mx 3m.yanafaa kwa kupanda miche. Matatu au
  majaruba yanarahisisha umwagiliaji, palizi na unyunyiziaji wa dawa.
  2
  Kupandikiza miche shambani na matumizi ya mbolea
  Weka samadi debe 2 au mbolea ya TSP au DAP kwenye tuta au jaruba na kuchanganya na
  udongo. Mbolea kiasi cha mifuko 2 TSP au DAP kwa hekta au ¾ mfuko kwa eka moja
  inashauriwa. Chagua miche yenye afya, majani na mizizi ya ipunguzwe ili kurahisisha upandaji.
  Panda miche kwenye mistari kwa nafasi ya sm 20 toka mstari hadi mstari, na miche hadi mche
  kwa nafasi ya sm 8 au sm 10. Tumia kijiti au kitu chochote chenye ncha kuchimba vijishimo
  vya kupandia miche. Mwagilia maji ya kutosha kila siku hasa sehemu zenye jua kali. Mbolea ya
  kukuzia CAN kiasi cha mifuko 2 kwa hekta au ¾ mfuko kwa eka moja iwekwe wiki mbili baada
  ya kupandikiza miche. Matumizi ya mbolea ya CAN yanataka uangalifu sana. Mbolea ikizidi
  hufanya mimea kuwa teketeke, shingo ya vitunguu kuwa nene, kuchelewesha kukoma na
  kupunguza mazao na ubora wa vitunguu. Pia kuoza kwa vitunguu ghalani kunaongezeka
  Kuzuia magugu
  Miche ya vitungguu, huota taratibu sana, hivyo miezi ya mwanzoni, miche husongwa sana na
  magugu. Palizi mbili mpaka tatu zinashauriwa na zinatosha kuweka shamba safi. Matumizi ya
  dawa za magugu ni madogo lakini dawa zinazoshauriwa ni pamoja na Alachlor na Oxyflourfen
  (Goal 2E). Hizi dawa ni nzuri kwani zina uwezo wa kuua magugu aina mbalimbali. Dawa
  inapuliziwa wiki mbili mpaka tatu baada ya kupandikiza miche shambani. Palizi baada ya
  kutumia dawa ya magugu ni muhimu ili kuondoa magugu sugu na pia kutifulia vitunguu.
  Wakati wa palizi, vitunguu na mizizi iliyowazi ifunikwe kwa udongo ili kuzuia jua lisiunguze
  mizizi au kubabua vitunguu.

  2.2 Magonjwa na wadudu waharibifu
  Vitunguu vinashambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali na kusababisha upungufu na
  ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo kwanza shamba likaguliwe mara kwa mara kuona dalili za
  mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua hatua za kuzuia kabla uharibifu
  mkubwa haujatokea.
  2.2.1 Magonjwa
  a) Baka zambarau (Puple Blotch)
  Ungonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi). Chanzo kikubwa cha ugonjwa ni mbegu zenye
  ugonjwa. Pia ugonjwa unajitokeza wakati kuna ukungu na unyevunyegu mwingi hewani has
  wakati wa masika. Kiasi cha 60-80 % ya mazao yanaweza kupotea kama ugonjwa
  hautadhibitiwa. Dalili za ugonjwa ni:-
  · kujitokeza madoa meupe yaliyodidimia kwenye majani na kwenye mashina ya mbegu
  · rangi ya zambarau kuwepo katikati ya doa jeupe.
  · majani kuanguka
  · mashina ya mbegu kuanguka kabla ya mbegu kutengenezwa
  Njia za kudhibiti:-
  · kupanda mbegu safi

  · kupanda vitunguu kwa kutumia mzunguko wa mazao
  · kuteketeza msalii ya vitunguu baada ya kuvuna
  · kupulizia dawa zilizopendekezwa kama Dithane M45 na Ridomil MZ. Dawa hizi
  zinachanganywa na povu la sabuni ili zijishike kwenye majani.
  b) Ubwiri vinyoya (Downy Mildew)
  Ugonjwa huu unasababishwa na kuvu (fangasi) na kuenezwa na mbegu, hewa na masalia ya
  vitunguu. Unajitokeza wakati kuna unyevunyevu mwingi hewani hasa wakati wa masika na
  dalili zake ni kama zifuatazo:-
  · madoa yenye umbo la yai, rangi ya njano iliyofifia hujitokeza kwenye majani makukuu
  na kusambaa mpaka kwenye majani machanga.
  · baada ya siku chache madoa ya njano yanafunikwa na ukungu wa rangi ya kijivu.
  · majani yanasinyaa na kufa kuanzia kwenye ncha.
  · shina la mbegu huzungukwa na vidonda na kusababisha kichwa cha mbegu kuanguka.
  Njia za kudhibiti ugonjwa ni kama zifuatavyo:-
  · kupanda mbegu safi
  · kupanda vitunguu kufuata mzunguko wa mazao
  · kupulizia dawa za ukungu kama dithane m45 na ridomil mz.
  · kuweka shamba safi
  · kuteketeza mabaki ya vitunguu
  · kumwagiliaji maji nyakati za asubuhi au jioni
  c) Kinyausi (Damping – off)
  Ugonjwa huu unasababishwa na fangasi na kuenezwa na udongo, mbegu na masalia ya mazao.
  Ugonjwa huu unasababisha mbegu kuoza kabla ya kuota na kunjauka kwa miche baada ya kuota.
  Ugonjwa unajitokeza hasa kitaluni ikiwa hali ya hewa ina unyevunyevu na udongo una maji
  maji.
  Njia za kudhibiti ni kama zifuatazo:-
  · mbegu ziwe safi na ziwekwe dawa ya thiram
  · kutumia mzunguko wa mazao
  · kusia mbegu kwa nafasi za kutosha
  · kuepukana na kubananisha miche kitaluni
  · kuepukanana na kumwagilia maji wakati wa jua kali au wakati kuna ukungu
  d) Virusi njano vya vitunguu (Onion yellow Dwarf virus)
  · Ugonjwa huu unasababishwa na virusi na kuenezwa na wadudu aina ya vidukari (wadudu
  mafuta). Dalili za ugonjwa ni:-
  · mistari ya rangi ya manjano kwenye majani.
  · kujikunja kwa majani
  · majani kugeuka rangi ya manjano na kuanguka
  · mimea mzima kudumaa, kujikunja na kufa.
  Njia za kudhibiti ugonjwa huu ni:-
  · kutumia mbegu safi
  · kuweka shamba katika hali ya usafi

  · kuzuia wadudu kwa kupulizia dawa kama selecron, actellic, dursban nk.

  2.2.2 Wadudu
  Wadudu wanaosababisha uharibifu mkubwa kwenye vitunguu ni chawa wekundu (thrips) na sota
  (cutworms). Wadudu wengine ni pamoja na utitiri wekundu (red spider mites) na vipekecha
  majani (leaf miner)
  a. Wadudu chawa (thrips)
  Uharibifu uletwao na wadudu chawa, unatofautiana msimu mmoja na mwingine kutegemeana na
  hali ya hewa. Mvua kidogo pamoja na joto kali unasababisha mlipuko wa wadudu.
  Wanshambulia majani kwa kukwaruakwarua na kunyonya maji hivyo kusababisha majani kuwa
  na rangi ya fedha/siliver na baadaye majani yanakauka. Upungufu mkubwa wa mazao unatokea.
  Njia ya kudhibiti hawa wadudu ni:-
  · kuweka shamba katika hali ya usafi
  · kuondoa magugu shambani na yanayozunguka shamba la vitunguu
  · kupulizia dawa ya wadudu kama karate, selecron, dursban, actellic.
  b. Sota (Cutworms)
  Sota au viwavi wa nondo wanasababisha uharibifu mkubwa. Viwavi wanakata mashina ya miche
  michanga sehemu ya chini ya shina juu ya ardhi. Sota wanapendelea kula wakati wa usiku na
  mchana kujificha kwenye ardhi karibu sana na sehemu waliokata shina. Uharibifu huu
  unapunguza sana idadi ya mimea shambani na kuleta upungufu wa mazao.
  Wadudu hawa wanadhibitiwa kwa kupulizia dawa kama; Karate Dursban na Actellic na kuweka
  shamba katika hali ya usafi.
  c. Utitiri wekundu (Red spider mites)
  Hawa ni wadudu wadogo sana, ambao wanajificha upande wa chini wa majani. Wanafyonza
  maji maji kwenye majani na kusababisha majani kuwa na rangi nyeupe. Wadudu hawa
  wanatengeneza utando mweupe kuzunguka majani na mashina. Mmea unashindwa kutengeneza
  chakula na baadaye inakufa.
  Njia ya kudhibiti:
  · kupulizia dawa za wadudu Karate na Selecron.
  · kuteketeza masalia ya mazao
  · kutumia mzunguko wa mazao
  d. Vipekecha majani (leaf miner)
  Hawa ni aina ya inzi wadogo, ambao viwavi wake wanashambulia majani, kwa kupekecha na
  kutengeneza mitandao wa mitaro kwenye majani. Viwavi wanashambulia majani na
  kusababisha majani kukauka. Upungufu mkubwa wa mazao hutokea.
  Njia ya dhibiti:
  · kupulizia dawa ya wadudu kama karate Selecron na Dursban
  · kuteketeza masalia ya mazao
  · kutumia mzunguko wa mazao  3.0 Kuvuna na hifadhi ya vitunguu
  Kabla ya kuvuna vitunguu kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa.

  Dalili ya vitunguu kukomaa ni:-
  · majani kunyauka na kuanza kukauka
  · asilimia 75 -100% kuangusha shingo na majani kukauka.

  3.1 Kuvuna
  Vitunguu vinavunwa kwa mikono. Mimea inangolewa au kuchimbuliwa kwa kutumia rato
  (jembe uma). Baada ya kuvuna vitunguu vinaweza kuachwa shambani vikiwa vimefunikwa na
  majani kukinga jua kali kwa muda wa siku mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa. Lengo ni
  kuimarisha ngozi ya vitunguu na kufanya michubuko na majeraha madogo madogo yanayotokea
  wakati wa kuvuna kuwa magumu na kutengeneza mokovu ambayo yanazuia vimelea vya
  magonjwa kuingia ndani. Pia kupunguza unyevu kwenye majani na mashina na kuruhusu
  sehemu ya chini ya shingo kufunga. Ikiwa usalama ni mdogo, vitunguu vinachambuliwa na
  kukatwa majani na mizizi na kuanikwa sehemu nyingine.

  3.2 Kuchambua
  · Tenga vitunguu vilivyooza, kuchubuka na kupasuka. Vitunguu vizuri vikaushwe peke
  yake.
  · Iwapo vitunguu vitahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye chaga, basi shingo zisikatwe, bali
  zisukwe na kufungwa pamoja, na kuninginizwa
  3.3 Kukausha
  Hatua hii ni muhimu ili kupunguza unyevu, kufanya vitunguu viwe vigumu na kuwa katika hali
  ya kulala bwete.Vitunguu vinaweza kukaushwa kwa kuninginiza kwenye chaga zilizopangwa
  mfano wa dari ndani ya banda au kutandaza kwenye kichanja chenye kuruhusu mzunguko wa
  hewa pande zote, chini ya kivuli sehemu kavu. Epuka kukausha vitunguu chini kwenye aridhini
  na hasa sehemu zenye jua kali. Jua linababusha vitunguu na kusababisha uharibifu. Ukaushaji
  huchukua muda wa siku 7 au zaidi kutegemeana na hali ya hewa.

  3.4 Kupanga madaraja
  Vitunguu vinachambuliwa tena baada ya kukausha ili kuondoa vitunguu vyote vyenye ugonjwa
  au dalili za ugonjwa, vilivyoota na kutoa mizizi na vyenye shingo nene. Vitunguu vinapangwa
  kwenye madaraja mbalimbali kufuata ukubwa, umbo au rangi. Hii inawezesha kuapta soko zuri
  na kuepukana na upotevu mkubwa wakati wa kuhifadhi.

  3.5 Kufungasha na kuweka vitambulisho
  Vifungashio vinavyopatikana ni mifuko ya nyavu vyenye uwezo wa ujazo wa kilo 20 au
  magunia ya katani. Mifuko ya nyavu ina ujazo mdogo na pia inarahisisha ubebaji. Magunia ya
  katani yanatumika lakini yanaficha vitunguu visionekane pia vinachukua mzigo mzito na kuleta
  usumbufu wakati wa kupakia na kupakua.
  Vitambulisho vinawekwa kwenye vifungashio ili kusaidia wasafirishaji kujua mzigo ulikotoka
  na pia kutangaza bidhaa inayohusika kwenye masoko ya nje na ndani.
  Kwa soko la nje vitambulisho vinatakiwa na habari zifuatazo:
  · Jina la bidhaa mf. Vitunguu Mango’la Red
  · Uzito kamili mf. 20 kg
  · Jina na anwani ya mkulima au kikundi, jina na anwani ya msafirishaji

  · Jina la kijiji wilaya, Mkoa na nchi mf. Igurusi, Mbarali, Mbeya, Tanzania
  · Grade 1
  Kwa soko la ndani vitambulisho vinakuwa na habari zifuatazo:
  · Jina la bidhaa.mf.vitunguu Mango,la Red
  · Uzito kamili mf. 20 kg
  · Jina la mkulima au kikundi na anwani John Geda au Jitegemee, Box 200, Mbarali
  Mbeya
  · Jina na anwani ya msambazaji mf:Mr. Saidi Mbaga Box 670, Mbeya

  3.6 Kusafirishaji
  Uangalifu wakati wa kupakia, kusafirisha na kupakua ni muhimu ili kuepukana na uharibifu na
  upotevu wa vitunguu. Mara nyingi vitunguu vinaharibika kutokana na ujazo kupita kiasi kwenye
  vifungashio na vyombo vya usafiri, pia kutokana na upakiaji na mpangilio mbaya, ambao
  unasababisha ugandamizaji na kubonyea kwa vitunguu. Wakati wa usafirishaji yafuatayo
  yazingatiwe:-
  · kutumia vyombo vya usafiri vinavyofaa hasa magari yenye nafasi ya kutosha na yenye
  kupitisha hewa
  · kupanga mifuko katika tabaka zenye safu zisizodi tatu
  · mifuko isitupwe wakati wa kupakia na kupakua
  · vitunguu visichanganywe na mazao mengine.

  3.7 Kuhifadhi

  Vitunguu vinahifadhiwa kwenye maghala bora kama kribu au mabanda ambayo yanaruhusu
  hewa na paa kuezekwa kwa manyasi ili kupunguza joto.
  Hifadhi kwenye kribu
  Kribu inajengwa kwa fito au mianzi na kuinuliwa juu mita moja toka usawa wa aridhi. Upana
  wa kribu uwe kati ya sm 60 na 150 ili kuruhusu upepo kupita kwa urahisi. Upepo unaondoa
  unyevu na joto kwenye vitunguu. Kribu igawanywe sehemu mbili zenye kina cha sm 60 kila
  moja na kutenganishwa na uwazi was m 30, ili kuruhusu mzunguko wa hewa. Wakati wa
  kutengeneza kribu yaafutayo yazingatiwe:-
  · Kribu ijengwe kwenye sehemu yenye upepo
  · Kribu iezekwe kwa nyasi ili kudhibiti joto na jua
  · Miguu ya kribi iwekwe vizuizi vya panya.
  · Weka vutunguu tabaka mbili na kina cha vitunguu kisizidi sm 60
  Hifadhi kwa kuninginiza vitunguu kwenye banda
  Hili ni banda lenye uwazi mkubwa, lenye upana usiozidi mita tano, na urefu toka chini hadi
  juu usizidi mita 2½. Banda linajengwa kwa miti, fito, mbao au mianzi na vitunguu
  vinahifadhiwa kwa kuninginiza kwenye fremu za fito ndani ya banda. Safu za vitunguu
  hupangwa kufuata urefu wa banda na kimo cha banda. Urefu wa banda huelekezw a kwenye
  mkondo wa upepo ili kuruhusu upepo kuingia na kutoka. Banda liezekwe kwa nyasi ili
  kudhibiti joto na jua. Kribu au banda vinahifadhi vitunguu vizuri kwa muda wa miezi sita
  bila kuharibika.

  3. 8. Upotevu wa vitunguu ghalani
  Vitunguu vingi hupotea wakati wa kuhifadhi kwa sababu ya:-
  · Kuoza
  · Kuota (toa majani na mizizi)
  · Kupoteza uzito

  3.8.1. Kuoza
  Kuoza kwa vitunguu vikiwa ghalani kunasababishwa na vimeliea vya fangasi au bacteia. Joto
  pamoja na unyevunyevu ndani ya ghala, kunasababisha kuzaliana na kuongezeka kwa vimelea
  vya magonjwa
  Kudhibiti:
  · Weka ghala katika hali ya usafi, kausha vizuri na chambua vitunguu ili kabla ya
  kuhifadhi.
  a ) Muozo Kitako (Bottom rot or basal rot)
  Vimelea vya aina ya fungus vinavyoishi kwenye udongo, vinashambulia sehemu ya chini ya
  vitunguu. Vimelea vinapenya kwenye sehemu zenye michubuko, inayotokea wakati wa palizi,
  kuvuna au kusafirishwa. Vitunguu vinaoza na baadaye vinakauka na kusinyaa. Njia zifuatazo
  zinadhibiti:-
  · mzunguko wa mazao
  · kuchambuaji mzuri kabla ya kuhifadhi
  · kuepuka michubuko wakati wa palizi na kuvuna
  b) Ukungu mweusi (Black mould).
  Ugonjwa huu unaletwa na vimelea vya fangasi, vinavyoishi kwenye udongo. Vimelea
  vinazaliana katikati ya maganda na ukungu mweusi kama poda unaonekana. Baadaye maganda
  yanasinyaa na kuvunjika.
  Kudhibiti
  · kutumia mzunguko wa mazao
  · kukagua ghala mara kwa mara na kuondoa vitunguu vilivyooza
  · kuweka ghala katika hali ya usafi.
  · Kuondoa masalia ya vitunguu na kuchoma moto.
  c) Kuoza shingo (Neck rot)
  Vimelea vya fangasi vinashambulia vitunguu vikiwa shambani kabla ya kuvuna. Ugonjwa
  hauonekani mpaka vitunguu vikomae, vivunwe, vikaushwe na kuhifadhiwa ghalani, ndipo
  ugonjwa hujitokeza. Ugonjwa unasababisha kuoza kwa vitunguu. Maganda ya vitunguu
  yanalainika kuanzia shingoni na nyama ya kitunguu huwa na sura ya maji maji. Vitunguu
  vilivyooza vinyauka na kusinyaa.
  Kudhibiti;
  · kukausha vitunguu vizuri kabla ya kuhifadhi
  · kuchoma na kuharibu masalia ya vitunguu shambani na ghalani.
  d) Muozo laini (Bacterial soft rot)
  8
  Ugonjwa unasababishwa na vimelea vya bacteria. Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kulainika
  kwa vitunguu na kutoa harufu mbaya. Ukiminya kitunguu maji yenye harufu mbaya yanatoka
  kwenye shingo. Muozo laini unatokea wakati hali ya hewa ikiwa na unyevunyevu na jotoi. Pia
  vitunguu vyenye shingo nene ambavyo havijakauka vizuri ni sehemu nzuri sana ya vimelea
  kuzaliana.
  Kudhibiti :
  · Ukaushaji wa haraka na wa uhakika baada ya kuvuna unapunguza sana ugonjwa huu

  3.8.2 Kuota na kupoteza uzito wa vitunguu
  Vitunguu vinakuwa katika hali ya kulala bwete bila kuota kwa zaidi ya miezi sita ikiwa hali ya
  hewa ghalani ni nzuri. Unyevunyevu mwingi ghalani ni adui mkubwa wa vitunguu
  vilivyohifadhiwa kwani inasababisha kuota kwa majani na mizizi. Pia hewa ikiwa kavu sana
  vitunguu hupoteza maji upesi na kusinyaa. Kuongezaka kwa joto na unyevunyevu ndani ya ghala
  kutokana na mzunguko mbaya wa hewa, uchafu ghalani, ukaushaji na uchambuaji mbaya
  vinasababisha uharibifu kubwa wa vitunguu ghalani
  Kudhibiti ;
  · ghala liwe safi pia liwe na uwezo wa kupitisha hewa kavu na ubaridi wa kutosha.
  · ghala lijengwe sehemu yenye upepo na kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa.
  · vifungashio vya vitunguu vipangwe vizuri ili kuruhusu hewa kupita juu na chini.
  · vitunguu ndani ya kribu/ghala vijazwe kina cha sentimeta 30-50.
  · vitunguu vichambuliwe vizuri kabla ya kuhifadhi.
  · vitunguu ghalani vikaguliwe mara kwa mara ili kuondoa vitunguu vilivyoharibika

  4.0 Uuzaji wa vitunguu
  Watu wa aina mabalimabali wanahusika na ununuzi na uuzaji wa vitunguu wakiwa ni pamoja na:
  wakulima, wachuuzi, wafanya biashara ndogondogo, wauza jumla, wauza rejareja, wasafirishaji
  na madalali. Ili koboresha uuzaji na kipato ni muhimu kuzingatia yafuatayo:
  · Kuboresha ujazo kwa kufuata vipimo vinavyokubalika (kufuta lumbesa
  · Kupeana habari za masoko na bei.
  · Kuboresha usafirishaji kwa kutumia vikundi.
  · Kuwepo na mtiririko wa kuuza vitungu mwaka mzima, kwa kuboresha hifadhi ikiwa
  ni pamoja na maghala.
  · Kutathimini na kuzingatia ubora wa vitunguu.
  · Kutathimini na kuboresha ufungashaji na usafirishaji
  Imeandaliwa na Mathias Kavishe

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: KILIMO NA HIFADHI BORA YA VITUNGUU Rating: 5 Reviewed By: Kilimo mifugo
  Scroll to Top