• Latest News

  Wednesday, December 3, 2014

  KILIMO BORA CHA NYANYA- MAGONJWA NA WADUDU
  Utangulizi
  Nyanya ni zao la chakula na biashara. Kilimo cha zao hili hufanyika majira yote
  (masika na kiangazi), na faida hupatikana haraka na ni ya kuridhisha ikilinganishwa
  na mazao mengine. Pamoja na umuhimu wa zao hili, wadudu waharibifu na
  magonjwa huathiri uzalishaji na ubora wa matunda. Ili mkulima aweze kupata faida
  na kuongeza pato la kaya yake ni vema kuzingatia udhibiti wa magonjwa na wadudu
  wa zao hili. Kipeperushi hiki kinatoa maelezo ya udhibiti wa magonjwa na wadudu
  muhimu ya zao la Nyanya.

  MAGONJWA YA NYANYA
  Bakajani chelewa (Late blight)
  Ugonjwa huu huenenzwa na vimelea vya fangasi. Husababishwa na hali ya hewa hasa
  ya unyevunyevu, na huenezwa na upepo. Majani, shina, matunda hushambuliwa.
  Majani huwa na ukungu mweupe na kijivu, na baadaye hukauka. Matunda huwa na
  mabaka ya kikahawia na baadaye kuoza. Mashina pia huwa na mabaka ya kikahawia.

  Udhibiti

  · Nyunyiza dawa ya kuzuia ukungu hasa wakati wa masika, Dawa
  zinazopendekezwa ni Ridomil, Dithane 45, Bravo, Funguran, milraz.
  · Fanya mzunguko wa mazao. Usipande nyanya sehemu moja kila msimu au
  palipolimwa mazao jamii ya nyanya km viazi mviringo, bilinganya, aina zote
  za pilipili na nyanya chungu.
  · Tumia mbegu safi
  · Panda aina za nyanya zinazovumilia ugomjwa
  Bakajani tangulia (Early blight)
  Huenezwa na vimelea vya fangasi. Husababishwa na kuenezwa na hali ya hewa
  pamoja na mbegu zenye ugonjwa. Mabaka ya kahawia yenye mistari ya mviringo
  huonekana kwenye majani na shina. Baka jeusi hutokea sehemu ya tunda
  inayoshikana na kikonyo.

  Udhibiti
  · Nyunyiza dawa ya Kocide, Funguran
  · Teketeza mabaka ya mazao baada ya kuvuna
  · Tumia mbegu safi na bora
  Mnyauko fusari (Fusarium wilt)
  Huenezwa na mbegu zenye ugonjwa. Husambazwa na vimelea vya fungasi
  vinavyoishi kwenye udongo.
  Ugonjwa hujitokeza zaidi wakati wa kiangazi. Vimelea hushambulia sehemu au
  mirija ya mmea ya kupitishia maji na chakula. Mmea hukosa maji na chakula na
  hatimaye hunyauka. Shina la mmea likipasuliwa ndani huonekana rangi ya kikahawia.

  Udhibiti
  · Tumia mbegu safi na bora
  · Tumia mzunguko wa mazao. Nyanya zisizungushwe na mazao jamii yake
  · Teketeza masalia ya mimea
  www.ariuyole.go.tz
  · Choma kitalu cha nyanya kabla ya kusia mbegu
  Mnyauko bacteria (Bacterial wilt)
  Ugonjwa husababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye udongo.
  Huenezwa na kusambazwa na mbegu na udongo wenye vimelea. Mirija ya mimea ya
  kupitishia maji na chakula hushambulia na mimea hunyauka ghafla. Mmea hukauka
  na kufa.

  Udhibiti
  · Panda mbegu safi
  · Panda nyanya sehemu ambayo haijawahi kupandwa viazi mviringo,
  bilinganya au nyanya chungu
  · Tumia mzunguko wa mazao
  · Hakikisha mfereji wa maji ya kumwagilia hayapiti kwenye shamba lenye
  historia ya ugonjwa huu.
  · Choma kitalu cha nyanya kabla ya kusia mbegu
  Mnyauko vetisili (Verticillum wilt)
  Hakuna dawa inayozuia au kutibu ugonjwa huu kwa sasa. Ugonjwa husababishwa na
  ukungu (fangasi) kwenye udongo. Ukungu huu huishi kwenye udongo kwa muda
  mrefu bila kudhurika. Ugonjwa huongezeka ikiwa mizimizi ya nyanya
  imeshambuliwa na minyo fundo; au kukiwepo na hali ya ubaridi au ukame. Ugonjwa
  husababisha hasara kubwa. Ugonjwa hushambulia sehemu ya ndani ya shina na
  kusababisha sehemu hiyo kuwa na rangi ya kijivu. Majani hugeuka njano na mimea
  kunyauka na kufa.

  Udhibiti
  · Tumia mzunguko wa mazao usiopungua miaka mine
  · Ondoa mabaki ya nyanya shambani
  · Tumia mbegu bora na safi
  Bakadoa (Bacterial spot)
  Ugonjwa huu huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu, pia
  kwenye hewa. Huenezwa kwa kasi sana wakati wa masika. Madoa ya rangi kahawia
  huonekana kwenye majani na matunda.

  Udhibiti
  · Panda mbegu bora na safi
  · Tumia mzunguko wa mazao
  · Teketeza masalia ya mazao
  · Nyunyizia dawa ya funguran, Kocide101, Cobox, Bravo
  Makovu bakteria (Bacterial canker)
  Ugonjwa huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu na hewani.
  Hutokea zaidi wakati wa masika. Majani hukauka nchani na makovu yaliyodidimia
  hutokea kwenye shina. Matunda huwa na makovu yenye rangi ya kahawia sehemu ya
  katikati.

  Udhibiti
  · Tumia mbegu bora na safi
  www.ariuyole.go.tz 2
  · Teketeza masalia ya mazao
  · Tumia mzunguko wa mazao
  Rasta (Yellow leaf curl)
  Ugonjwa huu husababishwa na virusi na huenezwa na nzi wadogo weupe. Hutokea
  zaidi wakati wa kiangazi. Mimea hudumaa na majani yaliyoshambuliwa huwa na
  rangi ya manjano na pengine rangi ya zambarau. Nyanya hupasuka.

  Udhibiti
  · Nyunyiza dawa za sumu za kuua wadudu (Selecron, Dursburn, Actelic)
  · Ng’oa mimea yenye ugonjwa
  · Tumia mzunguko wa mazao
  · Weka shamba katika hali ya usafi
  Batobato (Tomato mosaic virus)
  Ugonjwa husababishwa na virusi na hueezwa na mbegu na kugusana. Majani huwa na
  mchanganyiko wa rangi hasa kijani kibichi na kijani kilichofifia (majano). Majani
  hujikunja na manjani machanga huwa na maumbile yasiyo kawaida. Ukifikisha jani
  huwa linavinjikavunjika.

  Udhibiti
  · Tumia mbegu bora na safi
  · Ng’oa mimea iliyoshambuliwa
  · Teketeza masalia ya mazao
  · Weka shamba katika hali ya usafi  WADUDU WAHARIBIFU
  Viwavi Matunda (Fruit worm)
  Viwavi hawa hutokana na wadudu nondo. Viwavi hutoboa matunda na kuacha
  matundu na hatimaye matunda huoza. Hupunguza ubora wa matunda.

  Udhibiti
  Nyunyizia dawa ya kuua wadudu. Dawa hizo ni pamoja na Actelic 50EC, Selectron,
  Dursbaan, Maji ya majani ya mwarobaini au utupa pia huua wadudu.
  Utitiri wekundu (Red Spider mites)
  Hawa ni wadudu wekundu, wadogo sana wanaoweka utando chini ya majani, hasa
  wakati wa kiangazi. Wadudu hawa hufyonza utomvu kwenye majani na kusababisha
  majani kukauka.

  Udhibiti
  · Nyunyizia dawa za sumu. Dawa hizo ni pamoja na Actellic, Selecron,
  Dursbarn na Thionex
  · Mwagilia maji mara kwa mara
  · Weka shamba katika hali ya usafi
  www.ariuyole.go.tz 3
  Inzi weupe (White flies)
  Hawa ni Inzi weupe wadogo sana. Hujitokeza sana wakati wa kiangazi. Hueneza
  ugonjwa wa virusi ujulikanao kama Rasta.

  Udhibiti
  Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Selecron, Actellic, Dursban na
  thionex. Pia maji ya majani ya mwarobaini na utupa.
  Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)
  Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na
  kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea na kushindwa kuzaa
  matunda

  Udhibiti
  Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban
  maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.
  Minyoo (Nematodes)
  Ni minyoo midogomidogo ambayo hushambulia mizizi na kuweka vifundo. Mizizi
  hushindwa kuchukua maji na chakula kwenye udongo. Mimea hudumaa na
  kushindwa kuzaa

  Udhibiti
  · Tumia mzunguko wa mazao
  · Choma udongo wa kitalu kabla ya kusia mbegu kwa kutumia karatasi la
  plastiki jeusi na nishati ya jua
  · Choma masalia ya mazao
  Sota (Cutworms)
  Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wa
  mchana hujificha kwenye udongo na usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina
  usawa wa udongo.

  Udhibiti
  · Nyunyiza dawa za kuua wadudu kwenye shina usawa wa udongo
  · Hakikisha miche inapata maji ya kutosha.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: KILIMO BORA CHA NYANYA- MAGONJWA NA WADUDU Rating: 5 Reviewed By: Kilimo mifugo
  Scroll to Top