• Latest News

  Thursday, January 19, 2017

  UFUGAJI WA SAMAKI HATUA KWA HATUA :HATUA YA NNE

  Inaendelea...............
   Kama ulipitwa na Hatua ya Tatu Rejea Hatua ya tatu bofya hapa
  ULISHAJI NA UTUNZAJI WA SAMAKI BWAWANI
  Katika hatua hiyo tuliona kuwa vifaranga kabla ya kusafirishwa viwekwe kwenye vibwawa vidogo vidogo kwa muda wa kati ya saa 24 hadi 72 bila chakula ili kuzuia visichafue maji kwa kinyesi wakati vinasafirishwa, vifaranga visimwagwe wala kuruhusiwa kuingia kwenye bwawa wakati wa upandikizaji hadi mfugaji aruhusu maji yaliyomo kwenye chombo cha kusafirishia yabadilishane joto na  yale ya bwawani, na uandaaji na usafirishaji wa vifaranga ni vema ukafanywa muda ambao hali ya hewa inakuwa na ubaridi.
  Katika sehemu hii ya 5 tunaangalia hatua ya 4 ambayo ni ulishaji na utunzaji wa samaki bwawani. Samaki kama viumbehai wengine Huhitaji chakula ili waweze kukua na kuzaliana kwa wingi.  Hapa Dr. Berno Mnembuka mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA anashauri samaki  wapewe chakula angalau mara 2 kwa siku na muda unaopendekezwa ni saa 3 hadi 4 asubuhi  na saa 9 hadi 10 jioni kwa sababu muda huo maji yanakuwa na hewa ya kutosha ambayo inasaidia mmeng’enyo wa chakula kwa samaki.
  Jambo lingine la kufanya kwenye ulishaji wa samaki ni kuwapa vyakula tofauti kutegemeana na silka ya aina ya samaki unaowafuga. Kuna samaki wanaofaidika na vyakula vya nyama nyama kama vile kambale na sangara (hawa hawali pumba) na kuna samaki wengine kama sato wanakula vyakula mchanganyiko wa nyama na mboga mboga na wapo wengine wanaokula vyakula vyenye asili ya mimea tu ambao kitaalamu wanajulikana kwa jina la carps.
  Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Wanyama SUA, Dr. Mnembuka  pia anasema kuwa samaki wanapokuwa bwawani wanatumia hewa ambayo huyeyuka ndani ya maji, kiwango cha hewa hiyo kikipungua sana samaki hushindwa kula na kikizidi sana maana yake ukijani unakuwa mwingi ndani ya maji hivyo samaki hushindwa kuona na kuleta athari kwenye ulaji wake wa chakula. Kutokana na ukweli huo inashauriwa kukagua kiwango cha hewa kilichopo kwenye maji angalau mara 2 kwa wiki. Vifaa vya kufanyia ukaguzi vipo na vinapatikana katika maduka mbalimbali.
  Pamoja na kuangalia kiwango hicho cha hewa pia maji yanatakiwa yakaguliwe dhidi ya hewa chafu mfano kiasi cha tindikali au kiasi cha chumvi chumvi kilichopo kwenye maji, vile vile ukaguzi ufanywe dhidi ya taka ngumu kwa kutumia vipimo maalum ambavyo vinaweza kugundua hewa chafu iliyopo bwawani, lakini yote kwa yote kilelezo cha ubora wa maji ni samaki mwenyewe, anachotakiwa mfugaji ni kuwa karibu na mifugo yake ili aweze kubaini kwa haraka mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika mifugo yake.
  Hadi hapo tumefikia tamati ya sehemu ya 5 iliyozungumzia  hatua ya 4 ya ufugaji wa samaki ambayo ni ulishaji na utunzaji wa samaki bwawani. Jambo kubwa lililosisitizwa ni kuhakikisha samaki wanapewa chakula angalau mara 2 kwa siku ili uweze kuvuna samaki wenye tija ambao watakuwezesha kupata faida.
  Usikose kufuatilia sehemu ya 6 ambayo itakuwa ikizungumzia hatua ya 5 ya ufugaji wa samaki ambayo ni uvunaji na uhifadhi wa samaki
  Inaendelea.....................
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: UFUGAJI WA SAMAKI HATUA KWA HATUA :HATUA YA NNE Rating: 5 Reviewed By: Kilimo mifugo
  Scroll to Top